Header Ads

LightBlog

TUSOME WOTE, TUSIKIKE WOTE




Rafiki yangu amenipelekea andishi hili. Nimelisoma. Naona niliweke hapa nawe uweze kulisoma. Haya!


Wanaopaswa kuwa gerezani, 
nao wanatafuta urais?


Na Lawrence Kilimwiko*

NANI wanataka kuwa rais nchini Tanzania? Wana nini? Historia yao ikoje? Wanaishi maisha ya kiwango gani? Wana mali kiasi gani au ni masikini kiasi gani? Wanalipa kodi au ni wakwepa kodi?

Nani anafahamu yeyote anayetaka kugombea urais ili atupe taarifa na ikiwezekana atusaidie kujibu maswali yaliyoulizwa hapo juu?

Tanzania inaingia katika uchaguzi mkuu wa 2015 ikiwa katika mazingira yanayohitaji uchunguzi na uchambuzi wa aina ya kipekee.

Kuna watuhumiwa wa makosa makubwa, ukiwemo ukwapuaji Benki Kuu (BoT) wa zaidi ya shilingi bilioni 290. Unaitwa kashfa ya  EPA. Kuna uwindaji haramu wa tembo na faru na usafirishaji nje ya nchi wanyama hai kutoka mbugani. Kuna uzawadiaji mikataba kama ule wa Richmond wa kufua umeme wa dharura ambao, hata hivyo, haukupatikana.

Kuna wafanyabiashara wakubwa wa  dawa za kulevya ambao Rais Jakaya Kikwete aliwahi kuliambia taifa kuwa ana orodha yao wote; lakini hajawahi kuiweka wazi hadi leo.

Kuna wezi wa fedha za umma kupitia akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya BoT. Hata watumishi wa ikulu wako kwenye orodha ya waliochotewa mamilioni ya shilingi.

Je, miongoni mwa wote hawa na wengine, hakuna anayetaka kugombea urais? Hakuna ambao wamejichomeka kwenye ulingo wa siasa ili kuepuka kushitakiwa; na sasa wanatafuta urais ili kuficha zaidi sura na ukwasi wao unaotokana na wizi, ukwapuaji na ujambazi kiuchumi?

Tanzania haiwezi kuwa tofauti. Angalia Italia. Silvio Berlusconi, waziri mkuu wa zamani wa Italia, ni mmoja wa mamilionea wa  ki-Italia aliyekuwa akimiliki utajiri wa thamani ya dola za Marekani 6.2 bilioni.

Historia yake inaonyesha kuwa alianza maisha akiwa mchezadisko kwenye vilabu vya pombe na vingine. Baadaye alisoma na kuhitimu sheria mwaka 1961.

Biashara zake zimo katika maeneo kadhaa kuanzia kampuni ya ujenzi, televisheni kubwa ya Telemilano na nyingine mbili, kampuni ya uchapaji magazeti ya Giomele, redio, Shirika la habari la Rai pamoja na kumiliki klabu maarufu ya kandanda ya A.C.Milan.

Mwaka 1993 Berlusconi alianzisha chama cha siasa cha Forza Italia na kujitumbukiza kwenye siasa. Alitambua mapema kabisa kuwa ili aweze kufanikisha malengo yake; na hasa kukwepa mkono wa sheria kutokana na kufanya biashara nyingi haramu, ilikuwa muhimu kwake kuingia katika siasa – ili apate mahali pa kujikinga.

Njama hizo zilimsaidia sana Berlusconi kukwepa mkono wa sheria kutokana na makosa ya kukwepa kodi, udanganyifu, rushwa na  hata ngono. Kwa ufupi, maisha ya Berlusconi yamejaa mchanganyiko wa sifa na kashfa.

Alikuwa waziri mkuu wa Italia kwa vipindi vitatu, na mtawala aliyekumbwa na kashfa nyingi na hata kuhukumiwa kwenda jela. Lakini hakuwahi kutumikia jela kutokana na kujificha kwenye kichaka cha siasa.

Hata hivyo, baada ya kukwepa kwenda jela kutokana na makosa ya rushwa, ubakaji, kukwepa kodi na udanganyifu; hatimaye alijikuta akining’inizwa baada ya kutiwa hatiani na mahakama kwa kosa la kukwepa kulipa kodi mwaka 2013.

Kama hiyo haitoshi, alihukumiwa pia adhabu ya miaka saba jela kutokana na kufanya ngono na “kahaba” aliye chini ya umri wa mtu mzima. Adhabu hiyo, hata hivyo, ilibadilishwa na kuwa ya kutumikia jamii kwa mwaka moja kutokana na umri wake mkubwa – miaka 77.

Hiki kilikuwa kitu kipya kabisa kwa raia wa Italia ambao walifikia kuamini kwamba Silvio Berlusconi haguswi na mkono wa sheria kutokana na ukubwa kisiasa na utajiri wake.

Nchini Tanzania, wenye utajiri mkubwa walianza kwa kujipenyeza kwenye michezo kupitia vilabu vikubwa. Ukweli ni kwamba kelele za wanachama na mashabiki wa klabu, huweza kumsetiri mwizi na hata kuhakikisha kuwa hakabiliwi na mkono wa sheria.

Baada ya kugundua mbinu hiyo inafanya kazi, inawezekana sasa kuna waliojiingiza katika siasa, tena kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) au vyama vingine.

Siyo siri kwamba wizi na ufisadi wote uliotajwa hapo juu, umo nchini Tanzania. Siyo siri kwamba wizi mkubwa umewahusu viongozi wa serikali ambayo inaongozwa na CCM.

Siyo siri kwamba miongoni mwa wanaotaka kugombea urais, Oktoba mwaka huu, tena kupitia CCM, wamo watuhumiwa wakuu wa ama hujuma, wizi  au ukwapuaji mabilioni ya shilingi kupitia wizara ya fedha na BoT.

Ripoti ya hivi karibuni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa fedha za serikali (CAG); inaonyesha kuwa serikali inatumia vibaya fedha inazopewa; inapoteza fedha, na watumishi wake waliokabidhiwa dhamana kuu, wanatafuna fedha kama njugu kutoka shamba la bibi!

Ni kula! Kula! Kula! Ni kula faida na ziada; na hatimaye kula mbegu; kana kwamba mwakani hakuna kupanda!

Kinachostua wananchi wengi wapenda nchi yao, ni kuona waliotajwa na CAG – na huwataja mwaka hadi mwaka –  kuwa watuhumiwa ubadhilifu, wezi moja kwa moja, wakwapuaji na, au waandaa mipango ya uhujumu uchumi; ni miongoni mwa wanaotangulia kutangaza kugombea urais na ubunge.

Yuko wapi mwandishi wa kuwaanika hao? Yuko wapi mwandishi wa kuwahoji?

Kwa wizi wa waziwazi alioanika CAG, kuna wanaopaswa kuwa jela wakati huu au wakati wa uchaguzi, Oktoba. Serikali inayowaajiri, inayowakinga, inayostahili kuwafukuza au kuwakamata na kuwashitaki, iko kimya.

Ni serikali hiyohiyo ya chama hichohicho, inayotuhumiwa na kushutumiwa na CAG ambayo inasimamia upatikanaji rais kutoka miongoni mwa watuhumiwa  - Chama Cha Mapinduzi.

Katika mazingira haya, hakika hakuna kulala – kwa upande wa CCM na serikali yake. Wanataka kuhakikisha kuwa anapatikana mgombea na labda baadaye, rais atakayefunika kombe ili mwanaharamu apite.

Wanataka rais aendelee kutoka katika chama chao – CCM – kilichojaa viongozi wa serikali wanaotuhumiwa na kushutumiwa kwa wizi na ufisadi wa viwango mbalimbali; kuanzia kijijini hadi ikulu.

Wanataka kuendelea kujenga kinga kwa wahalifu wanaowafahamu, waliowaweka madarakani, waliowalea na watakaoendelea kulinda, kuhifadhi na hata kuenzi genge la wezi wa tunda la jasho na damu ya Watanzania.

Chama Cha Mapinduzi kinaweza kufananishwa na mtu mmoja aitwaye Robert Mugabe, rais wa Zimbabwe, ambaye aliapa kufia ofisini kwa hofu ya kukamatwa na kushitakiwa, pale tu atakapotoka ikulu.

Kuiba fedha za umma, kushiriki kuiba, kuruhusu kuiba na, au kunyamazia kuiba, ni kosa kubwa kimaandili, kisiasa na kisheria.

Wizi usioadhibiwa, au usiokemewa; na badala yake ukawa wizi wa kuendeleza kwa “gharama yoyote ile,” alimradi mtu amebaki madarakani; ndio unafanya vyama na watawala watake kufia madarakani; kama inzi anavyofia kwenye kidonda. Hawaoni usalama wao nje ya madaraka ya dola.

Watajipitisha makanisani, misikitini, misibani, kwenye harusi na matanga; wakijifanya wacha-Mungu na wenye kuwahurumia wasumbukao kwa njaa, maradhi na kiu; wakiwalaghai watu kwa vitenge, kanga, pilau au kofia za chama au ahadi za ajira, ili wapate kubaki madarakani.

Hakika, Watanzania wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuacha ngonjera za kuthamini “uasisi” na “kuleta uhuru.” Siyo siri kwamba vyama vilivyopigania uhuru Afrika na kwingineko, vingi viliingiliwa na kirusi cha wizi na ufisadi na hatimaye kuangushwa na umma.

Tanzania siyo kisiwa! Watanzania wanaona, kusikia na kunusa. Kama mwizi wa mali yao hakamatwi, basi wasiomkamata wasiwaombe kura ya kuendelea kutawala. Au wakiwaomba kura, basi wawakatalie.

CCM haikuundwa ili ilee wezi, iwatukuzwe na iwaweke madarakani. Hapana! Kwa kauli za Mwalimu Nyerere, iliundwa kulinda na kudumisha uhuru wa nchi na raia wake; kusimamia haki na maendeleo ya wakulima na wafanyakazi, kuhakikisha kuwa matumizi ya utajiri wa taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi, na hasa jitihada za kuondosha ujinga, maradhi na umaskini.

Kama walioahidi na wanaopaswa kuamini hayo ndio wenye serikali inayoanikwa na CAG kuwa ni badhilifu kupindukia; basi wameandika barua ya maombi kwa umma wakitaka kufukuzwa kazi. Watafukuzwa!

Kuwafukuza kazi ni kutowachagua; lakini kwanza ni kuwataka wagombea wao, hasa wanaotaka urais, kutaja walikopata fedha wanazomwaga misibani, michezoni, misikitini na makanisani; na jinsi watakavyozirejesha.

Isemwe tu basi, kwamba CCM bado ina nafasi ya kujisahihisha kwa kuwaengua wagombea urais, ubunge na udiwani – wote  wasio waadilifu – wahujumu, wezi, matapeli, walafi, wababaishaji na mafisadi.

Kama hilo litaigharimu kushindwa katika uchaguzi mkuu huu, isiwe hoja. Wakae pembeni. Wajipange upya na kurudi kwenye misingi walioyiacha, ndipo warejee kwenye kinyang’anyiro wakiwa wasafi na wenye sifa ya kushindana na hata kushinda.

*Lawrence Kilimwiko ni mshauri wa habari na mwandishi wa vitabu kutoka asasi ya Interlstar Consults, Dar es Salaam: lkilimwiko2015@gmail.com, Mob. 0754 321308.

No comments

Powered by Blogger.