Header Ads

LightBlog

MTANZANIA WA KWANZA KUPANDA MLIMA EVEREST



MTANZANIA KWENYE KILELE CHA EVEREST

Ni Wilfred Moshi. 
Amekuwa Mtanzania wa kwanza kufika kilele cha mlima mrefu kuliko yote duniani.
 
Na Freddy Macha 
kwa ushirikiano wa Urban Pulse

KIJANA Wilfred Moshi, ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda mlima Everest - mlima mrefu kuliko yote duniani.

Huyu ni “Mbongo” wa kawaida tu, mzoefu wa kufanya kazi ya upagazi ya kuwahudumia watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro.

Hivi karibuni, Moshi alialikwa nchini Uingereza kutembelea shule mbalimbali za Scotland. Alikuwako kwa majuma matano na kuweza kukutana na takribani wanafunzi 5,000.

Wanafunzi walitaka kufahamu namna alivyopanda mlima Everest wenye mita 8,848 (futi 29, 029). Watu 4,000 wamewahi kupanda mlima huu mgumu kukwea kuliko yote duniani, tangu Edmund Hillary na Sherpa Tenzig Norgay walipofika kileleni mwaka 1953. Watu 200 kati ya waliokwea mlima huo walifariki.

Mwaka huu wanne wameshafariki wakijaribu shughuli hii inayochukua  miezi miwili na kugharimu Dola 100,000 (Shilingi milioni 157,500,000). Hapa, linganisha na Mlima Kilimanjaro unaopandwa kwa siku tano na kwa gharama (ikiwepo ya vifaa husika), Dola 2,000 (Shilingi milioni 3.1).

Wilfred Moshi ni Mtanzania wa kwanza na Mwafrika wa tatu kufikia kilele cha kitendawili hiki cha “Chomolungma” – jina la wenyeji kabla mlima huu haujabandikwa jina la Everest, enzi za ukoloni wa Uingereza.  Alikanyaga kileleni tarehe 19 Mei mwaka huu.

Wilfred alizaliwa mwaka 1979. Alimaliza Kidato cha VI shule ya Kilimanjaro Boys. Amekuwa akipanda Mlima Kilimanjaro tangu angali bado shuleni – akiwa na miaka 19.

Mara baada ya kuwasili Edinburgh, Scotland,  Wilfredalikaribishwa bungeni; akakutana na Waziri wa Sheria, Mheshimiwa Kenneth MacAskill na viongozi wengine. Safari hii ilikirimiwa na shirika la “Twende Pamoja” lililoanzishwa na Mike Knox miaka 30 iliyopita.

“Twende Pamoja” limejenga ushirikiano kati ya wanafunzi wa Scotland na shule 34  za Tanzania. Ni moja  ya mashirika, watu binafsi  na wafadhili mbalimbali duniani waliochangia fedha za kumwezesha Moshi kupanda mlima Everest.

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe, naye alisafiri toka London kumtembelea Wilfred Moshi na kumpa heko. Umbali wa London hadi Scotland ni kama Dar es Salaam na Kigoma.

Lakini kwanini Moshi anahusudu kupanda milima.

Yeye anasema, kwanza lengo lake lilikuwa kutimiza ndoto yake ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda Everest. Ameitimiza.

Pili, upandaji milima ni moja ya njia zinazoweza kusaidia kujenga jamii kwa misaada na fadhila za mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO). Tujiulize vipi alisaidiwa na watu wengi kuchanga fedha nyingi kiasi hicho.

Tatu, Moshi amethibitisha ukiwa na moyo na jitihada unaweza kufanya lolote. Ushujaa na ushupavu wake utasaidia kuwahamasisha Watanzania kuwa, ukitaka kufanya jambo lolote lile, unaweza ili mradi uwe na moyo na nidhamu.

Mpanda milima mashuhuri, Mike Hamill, aliyekwishafika vilele vyote vya milima mikubwa saba duniani, anasema katika kitabu chake kipya – Climbing Seven Summits –  kwamba wapanda milima ni watu wenye moyo wa kufikia malengo na kufanikiwa katika maisha yao.

Akiwa Uingereza, Moshi alipanda mlima wa Ben Nevis,  mrefu kuzidi yote katika nchi hii – wenye mita 1,344 (futi  4, 409).

Baada ya kuimudu milima mitatu, sasa Wilfred Moshi ameazimia kupanda milima katika mabara yote saba duniani. Anasema amebakisha milima ya Aconcagua (Marekani ya Kusini ), Kosciuszko (Australia), Vinson Massif (Antarctica), McKinley (Alaska) na  Elbrus (Urusi).

Mungu ambariki Mtanzania huyu mwenye hamasa na anayetuletea sifa.

Soma habari zaidi:
http://wilfredmoshi.wordpress.com/



2 comments

Madaraka said...

Tunampa pongezi nyingi. Kilimanjaro pekee inatutoa jasho. Everest itakuwa ni changamoto kubwa zaidi.

Unknown said...

Amefanya makubwa

Powered by Blogger.