Tunataka kuendelea kulinda uhuru wetu wa mawazo na uhuru wa kujieleza, kwani uhuru huo ni haki yetu. Na uhuru hauna kikomo, wala hakuna wakati tunapoweza kusema uhuru tulionao unatosha. Hapana. Kila hatua inazaa matakwa mapya ya uhuru wa binadamu.

Friday, January 29, 2016

FURSA ILIYOPOTEA?DK. SHEIN HAJUI JINSI YA
KUKUMBUKWA DAIMA?

Dk. Ali Mohamed Shein hajui jinsi ya kuandika historia isiyofutika. Hajui. Angekuwa anajua asingekuwa ameng’ang’ania kiti cha urais aliopoteza miezi mitatu iliyopita.

Katika mazingira tuliyomo, Dk. Shein aweza kusema na kutenda – kwamba:

1.  Asilazimishwe kuwa rais Zanzibar wakati anajua kuwa hakushinda. Aachie.

2.  Asichonganishwe na umma wa Zanzibar kwa kitu kinachopita; tena haraka. Aachie.

3.  Asifanywe kondoo wa kafara kwa madai ya kulinda umoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Aachie.


4.  Asifanywe chanzo cha mfarakano mkuu na hata umwagaji damu; eti kwa kuwa analinda uhai wa CCM Visiwani. Aachie.


5.  Asifanywe kinga ya wachochezi wa ubaguzi wa rangi na asili ya watokako. Aachie.


6.  Asifanywe mjinga, mpuuzi na mroho wa madaraka; kumbe wanaomsukuma ndio wenye maslahi mapana; hata ya kifisadi. Aachie.

7.  Asipoteze hadhi yake ya kisomo na utendaji katika kipindi chake chote cha uongozi; vyote vikaonekana kuwa si kitu. Aachie.

8.  Asifanywe kuwa mtu asiye na uwezo wa kufikiri – kuona, kusikia na kutenda inavyopasa – kwa mtu mstaarabu na mweledi. Aachie.

9.  Asifanane na walafi wa kale na kale wasemao hawawezi kuachia madaraka kwa madai kuwa hawajaona “mwingine anayefaa.” Upuunzi mtupu. Nani amewatafuta na kuwakosa. Aachie.


10.                   Asishindwe kuona mikono lukuki ya historia ikiwa imekunjuliwa, tayari kumpokea Dk. Shein na kumweka kwenye nafasi yake anayostahili na hata kuenziwa. Aachie.

11.                   Asikatae kushiriki kazi kuu ya kuepusha migogoro na hata vita; na papohapo kuwa balozi wa amani kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika. Aachie.


12.                   Asipoteze nafasi hii adimu ya kuwa kiongozi mwingine katika Afrika asiyeenda kwa nguvu za ulafi na tamaa isiyoelezeka ya ufalme wa kisiasa – angalia: Uganda, Kongo, Burundi, Rwanda, Zimbabwe – wengi tu. Wanataka na wanajigamba kuwa watafia kwenye kidonda kama inzi. Aachie.


13.                   Afahamu kuwa siyo kila wakati mihula ya utawala wa kisiasa huenda kwa hesabu za miaka. Anaweza akaingia leo akatoka kesho – kwa sababu mbalimbali nje ya uwezo wake, uwezo wangu; na bado nchi ikaendelea kuwapo. Aachie.

14.                   Afahamu kuwa maisha ya watu wa Zanzibar na Tanganyika, ndio muhimu zaidi kuliko maslahi ya CCM, viongozi wake maslahi yake binafsi. Aachie.


15.                   Ajue kuwa atakuwa mtu huru; anayetembea kifua mbele, anayeheshimika na anayepigiwa mfano; kuliko kutumiwa kama chambo au kichocheo cha vurugu, mifarakano na hata ukimbizi na umwagaji damu (kama ilivyowahi kuwa). Aachie.


Tutamwona wa hekima, heshima; na jasiri atendaye kwa manufaa ya wananchi wake na taifa lake; hata dunia yake. Akatae kuwa mkuki wa kuchomea wanaotafuta mwafaka kwa njia iliyokubaliwa kikatiba na kisheria – Uchaguzi. Aitikie sauti ya wapigakura wa Zanzibar. Ndio waamuzi wa kweli na pekee. Aachie ngazi .

Tanzania ya wapenda amani na utulivu itambeba. Afrika itamuenzi. Historia itamwandalia makao ya furaha kwa uhai wake wote uliosalia. 

Hata baada ya kifo chake – na kwa imani yake – roho yake itawekwa mahali panapostahili – bila shaka karibu na watu wake ambao atakuwa amekataza kusaliti.

Inawezekana. Huu ndio ufalme kuliko wa kinyang’au wa “sinzia nikumalize!” Dk. Shein upo?
nt.


Friday, January 1, 2016

NANI RAIS ZANZIBAR?Kutoka Meza ya 
Mhariri wa Jamii

Dk. Magufuli
anapomtaka 
Maalim Seif
‘apige kazi’
Zanzibar

 (Mwananchi, Januari 1, 2016)

Kutoka Meza ya 
Mhariri wa Jamii

Wiki iliyopita ilikuwa “Wiki ya Zanzibar.” Kwanini? Kwa sababu wapinzani wakuu wawili kisiasa Visiwani walikuwa Dar es Salaam.

Hao ni Ali Mohamed Shein na Maalim Seif Shariff.

Walikuwa Dar es Salaam kumweleza Rais Dk. John Magufuli jinsi mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa Zanzibar yanavyoendelea na hatua iliyofikiwa.

Tarehe 28 Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kufutwa kwa uchaguzi mkuu na matokeo yake Zanzibar.

Wakati Jecha anatangaza kufutwa kwa uchaguzi na matokeo yote, tayari matokeo ya majimbo 33 yalikuwa yametangazwa.

Hadi tangazo la kufuta uchaguzi, kila chama kilikuwa na viti 27 vya uwakilishi. CCM haikuwa imepata hata kiti kimoja kisiwani Pemba. CUF ilikuwa imenyakua viti tisa Unguja. Ngome kuu ya CUF ni Pemba.

Sasa kwanini mwenyekiti wa ZEC alifuta uchaguzi? Alidai kwamba kulikuwa na vurugu katika maeneo mbalimbali; kwamba yalijitokeza mazingira yaliyofanya uchaguzi usiwe huru na wa haki; kwamba Maalim Seif Shariff Hamad alijitangazia ushindi.

Sheria ya uchaguzi inatoa adhabu kwa mtu anayetangaza matokeo badala ya Tume. Je, Maalim Seif ameshitakiwa? Hakushitakiwa. Hajashitakiwa.

Sheria ya uchaguzi inatoa mamlaka kwa Tume kusimamisha au kuahirisha uchaguzi katika eneo ambako kuna tatizo. Je, kuna hatua yoyote iliyochukuliwa kule ambako inadaiwa kutokea vurugu? Hapana.

Jecha alifuta uchaguzi wote – ambako inadaiwa kuwa na vurugu na kule ambako kulikuwa na utulivu; na usalama.
                               
Sasa hili lina uhusiano gani na kwenda Dar es Salaam kwa wagombea wa vyama hasimu – CCM na CUF? Kuna mambo mawili makubwa:

Kwanza, mgombea wa CUF ambaye ni katibu mkuu wa chama chake na makamu wa kwanza wa rais katika serikali ya umoja wa kitaifa (SUK), Maalim Seif anashikilia kuwa uchaguzi ulifutwa baada ya yeye kuonekana ameshinda.

Maalim anabeba “makabrasha muhimu” yenye taarifa mbalimbali kuthitbitisha ushindi wake na chama chake. Anadai kufuta uchaguzi ni njama za kutaka kupora ushindi wa chama chake na wapigakura wa Zanzibar.

Pili, CCM inadai kuwa ufutaji matokeo ilikuwa hatua sahihi. Inataka sasa uchaguzi urudiwe.

CUF inakataa kurudia uchaguzi. Inadai siyo haki wala sahihi. Inataka ujumuishaji matokeo uendelee kutoka pale zoezi lilipositishwa.

Maalim Serif na CUF wanadai kuwa na  matokeo sahihi. King’ang’anizi chao kinatokana na kile wanachoita “zana za ukweli” – fomu za matokeo na zilizosainiwa kutoka vituoni.

Kuna madai kuwa CCM imekwisha jiimarisha kwa kuongeza idadi kubwa ya wapigakura Visiwani na ndio maana inataka uchaguzi urudiwe.

Inadaiwa walioongezeka ni watendaji katika chama hicho na serikalini; na askari polisi na JWTZ.

Katika mazingira haya, CCM imebanwa. Ina kitu mdomoni. Ikikitema itakuwa imetema utamu. Ikikimeza itakuwa imemeza moto. Kote kuna madhara.

Lakini ni kweli kwamba uchaguzi na matokeo yake yote vilifutwa? Hapana. Siyo kweli. Baadhi ya matokeo, ingawa yalitamkwa kufutwa, hayakufutika. Kuna walioyakingia kifua.

Baadhi ya waliochaguliwa kuwa wabunge wa bunge la Muungano, walikwenda Dodoma haraka na kuapishwa. Ni hao waliombeba mgombea urais wa Muungano kutoka upande wa pili wa Muungano.

Je, katika mazingira haya, uchaguzi ukirudiwa Zanzibar ina maana na hao walioko bungeni Dodoma watarudi kwenye kinyang’anyiro?

Kurudi katika uchaguzi ni kubatilisha ubunge wa Wazanzibari waliokwishaapa. Ni  kumwacha rais katika mgogoro mkubwa kisiasa na kikatiba – ambamo yumo tayari.

Kuendelea kuwa wabunge katika bunge la Muungano; huku Zanzibar wakirudia uchaguzi, ni kujinyima uhalali na hivyo kuonekana mamluki waliochukuliwa rasmi kuhalalisha matakwa ya CCM.

Rais Magufuli hawezi, kama ambavyo hastahili, kukubaliana na hili na bado akabaki kuonekana mwadilifu mbele ya Watanzania na jumuia ya kimataifa.

Kwanini? Kwa sababu uchaguzi uliobatilishwa hauwezi kuzaa wachache ambao sio batili. Na ili “waliobatili” wawe halali – ingawa awali walifanywa halali kwa shabaha maalumu – sharti ujumuishaji kura za uchaguzi wa Oktoba uendelee kutoka pale ulipositishwa.

Hii maana yake ni kwamba huwezi kurudia uchaguzi Zanzibar. Ama uchaguzi unaendelea kwa kujumuisha matokeo; au majumuisho yaliyopo (hadi kusitishwa kwa uchaguzi) yanachukuliwa kuwa ndio matokeo sahihi na halali ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Je, Rais Magufuli anaona “ukora” huu wa kisiasa Zanzibar? Je, anaweza kutema wabunge waliompa “uhalali” kwa kuwarejesha katika kukurukakara za kuomba kura?

Sikiliza kauli za marais Magufuli na Shein baada ya kikao cha Dar es Salaam.

Vyombo vya habari vilimnukuu Rais Magufuli akisema amehakikishiwa na Maalim Seif kuwaa wanaendelea vizuri katika mazungumzo; na kwamba amemtaka “…wakamalize majadiliano yao na apige kazi.” Ikulu haijakanusha.

Naye Dk. Shein alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari, “…mazungumzo yanaendelea vizuri na yatakapomalizika tutatoa taarifa kwa umma kuwaeleza maafikiano yaliyofikiwa.”

Kauli hizi mbili hazitofautiani. Kama Magufuli ana maana ya anachosema, na kwa misingi iliyoelezwa hapo juu; basi siyo tu hakuna sababu wala haja ya kurudia uchaguzi; bali hakuna uchaguzi.

ndi.

Sunday, July 5, 2015

Spika Makinda anafanya kazi ya nani?


Fastafasta ya serikali

Hii kazi ambayo Spika Anne Makinda anafanya; ni kazi ya shetani. Hakuna jina wala njia nyingine yoyote ya kuiita. Huku kutoa nje ya vikao (Ijumaa na Jumamosi), wabunge wanaopinga miswada ya kinyonyaji - ambayo ni wazi kabisa kwamba imebeba maslahi ya wanyakazi na siyo wananchi - iwe kwa msuko wa makusudi au bila kujua; ni kufanya "kazi chafu."

Hapa hakuna swala la vyama na itikadi za vyama. Hapa kuna maslahi ya nchi. Na Makinda, akiwa kiongozi wa Bunge, alipaswa kuelewa hili; kwamba miswada ya gesi, petroli na uwazi, siyo ya kupitisha bungeni kama mifugo inavyopitishwa kwenye josho. Inahitaji fikra pevu na muda wa kutosha. Basi kwa tendo lake, Makinda atakuwa anajua kilicho nyuma ya pazia; nyuma ya fastafasta - na hii yaweza kuwa ni kulinda mafao ya binafsi na siyo taifa na watu wake.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba wabunge wengi wa CCM, baada ya kuona wenzao wa upinzani wametolewa nje, wakaacha kujadili miswada hiyo; wakaanza kujadili na kulaani wabunge waliotolewa nje; wakaanza kupendekeza hatua kali zaidi dhidi ya waliotolewa nje; na wakaanza kuimba ngonjera za wasifu kwa spika aliyekosa ujasiri; akakosa ukomavu; akakosa maarifa na hekima. Shida!

Click here to go to my facebook page. 

Sunday, June 21, 2015

Hawakuandikishwa: wameachwa au wamekataa?

Kila mwananchi ana haki ya kujiadikisha ili aweze 
kushiriki uchaguzi katika eneo lake - Oktoba 2015. 


WOTE AMBAO HAWAKUANDIKISHWA  
KATIKA DAFTARI LA WAPIGAKURA
 WAWEZA KUJITOKEZA KUPITIA HAPA

Kwenye mawasiliano ya imeili mjadala unaendelea. Waandishi wa habari na wasio waandishi wanakusanya majina ya watu ambao hawakuandikishwa katika daftari la kupiga kura - kwa sababu zozote zile - katika maeneo ambako tayari Tume ya Uchaguzi imetangaza kuwa imekamilisha uandikishaji. TUWAFAHAMU WAO NA IDADI YAO. NAO WAFAHAMIANE.

Je, wewe unajua nani hakuandikishwa au anadai kutoandikishwa katika eneo lako? Tupe taarifa kwa mtindo huu hapa:

Unachoombwa kufanya:
1. Sikiliza.
2. Pata anayedai kuwa hakuandikishwa.
3. Pata majina yake matatu.
4. Pata anakoishi na anwani yake/simu yake.
5. Pata kitambulisho chake chochote – kama kipo.
6. Pata maelezo: Kwanini hakuandikishwa/mazingira.
7. Rekodi/nukuu kauli anazodai kuambiwa na waandikishaji.
8. Kama simu yako ina kamera, pata picha yake.
9. Peleka taarifa zako kwa:

       ndimara2014@gmail.com
10. Kwa maulizo zaidi ita: 0713 61 48 72.Maelekezo yaliyopelekwa kwa waandishi wa habari na wadau wa habari sehemu mbalimbali nchini ni kama ifuatavyo:

Kuwa Jicho, Sikio na Mdomo wa Jamii


OKTOBA mwaka huu (2015) kutakuwa na Uchaguzi Mkuu – kuchagua madiwani, wabunge na rais. Hivi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inafanya kazi ya kuandikisha wapigakura.

Tayari Tume imetangaza kumaliza kazi ya kuandikisha wapigakura katika baadhi ya wilaya; LAKINI tangazo hilo linafuatiwa mgongoni na sauti nyingi za wananchi wanaodai kuwa hawakuandikishwa.

Nani hakuandikishwa? Yuko wapi? Ana maelezo yapi kuhusu kutoandikishwa?

Katika eneo unamoishi au uliko sasa kikazi au kwa matembezi, kuna wananchi wanaodai kuwa Tume haikuwaandikisha. Wangependa kuandikishwa ili washiriki kuchagua viongozi wanaoona watawatumikia; au watakaowawajibisha pale watakaposhindwa kuwahudumia.

Moja ya kazi kuu za mwandishi wa habari ni kupaza sauti za wananchi; ili wanachofikiri, wanachotaka, wanachosema na wanachotenda au kutendewa, kiweze kusikika kwa wengine, wakiwemo wenye mamlaka na dola kwa jumla.

Ukiwa jicho la nyongeza la jamii; sikio la nyongeza la jamii; na mdomo wa nyongeza wa jamii; sasa tafuta na kurekodi, kwa manufaa ya umma na watawala; watu wote katika eneo ulipo au unakokwenda, ambao kilio chao ni kutoadikishwa.

Siyo rahisi kuorodhesha kila mmoja ambaye anadai kutoandikishwa; lakini una uwezo wa kufikia hadi watu 50 au zaidi ili kuweka ushahidi unaoweza kusaidia kuleta utatuzi na hata mabadiliko makubwa katika jamii. Ni heshima iliyoje kuwa mmoja wa vibarua wa umma na kutambuliwa hivyo!

Tuko waandishi saba. Tunakushirikisha wewe na mwishoni mwa kazi hii ya kujituma kukutana na wenyekilio na kukusanya taarifa hizi, utakuwa tayari sehemu ya kundi hili. 

Haya ni mazingira yaliyosheheni FURSA za kuinua na kuibua vipaji vya waandishi wa habari. Ni fursa za kutumikia umma kwa njia ya kurekodi ukweli, tena kuurekodi kwa usahihi; ili wahusika waweze kuchukua hatua. Ni fursa zinazozaa, kulea na kukomaza umahiri katika taaluma ya habari. 

Unachoombwa kufanya:

1.     Sikiliza.
2.     Pata anayedai kuwa hakuandikishwa.
3.     Pata majina yake matatu.
4.     Pata anakoishi na anwani yake/simu yake.
5.     Pata kitambulisho chake chochote – kama kipo.
6.     Pata maelezo: Kwanini hakuandikishwa/mazingira.
7.     Rekodi kauli anazodai kuambiwa na waandikishaji.
8.     Kama simu yako ina kamera, pata picha yake.
Peleka taarifa zako kwa ndimara2014@gmail.com
10.                        Kwa maulizo ita: 0713 61 48 72.
Asanteni,

Ndimara Tegambwage
 

Friday, May 29, 2015

TUSOME WOTE, TUSIKIKE WOTE
Rafiki yangu amenipelekea andishi hili. Nimelisoma. Naona niliweke hapa nawe uweze kulisoma. Haya!


Wanaopaswa kuwa gerezani, 
nao wanatafuta urais?


Na Lawrence Kilimwiko*

NANI wanataka kuwa rais nchini Tanzania? Wana nini? Historia yao ikoje? Wanaishi maisha ya kiwango gani? Wana mali kiasi gani au ni masikini kiasi gani? Wanalipa kodi au ni wakwepa kodi?

Nani anafahamu yeyote anayetaka kugombea urais ili atupe taarifa na ikiwezekana atusaidie kujibu maswali yaliyoulizwa hapo juu?

Tanzania inaingia katika uchaguzi mkuu wa 2015 ikiwa katika mazingira yanayohitaji uchunguzi na uchambuzi wa aina ya kipekee.

Kuna watuhumiwa wa makosa makubwa, ukiwemo ukwapuaji Benki Kuu (BoT) wa zaidi ya shilingi bilioni 290. Unaitwa kashfa ya  EPA. Kuna uwindaji haramu wa tembo na faru na usafirishaji nje ya nchi wanyama hai kutoka mbugani. Kuna uzawadiaji mikataba kama ule wa Richmond wa kufua umeme wa dharura ambao, hata hivyo, haukupatikana.

Kuna wafanyabiashara wakubwa wa  dawa za kulevya ambao Rais Jakaya Kikwete aliwahi kuliambia taifa kuwa ana orodha yao wote; lakini hajawahi kuiweka wazi hadi leo.

Kuna wezi wa fedha za umma kupitia akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya BoT. Hata watumishi wa ikulu wako kwenye orodha ya waliochotewa mamilioni ya shilingi.

Je, miongoni mwa wote hawa na wengine, hakuna anayetaka kugombea urais? Hakuna ambao wamejichomeka kwenye ulingo wa siasa ili kuepuka kushitakiwa; na sasa wanatafuta urais ili kuficha zaidi sura na ukwasi wao unaotokana na wizi, ukwapuaji na ujambazi kiuchumi?

Tanzania haiwezi kuwa tofauti. Angalia Italia. Silvio Berlusconi, waziri mkuu wa zamani wa Italia, ni mmoja wa mamilionea wa  ki-Italia aliyekuwa akimiliki utajiri wa thamani ya dola za Marekani 6.2 bilioni.

Historia yake inaonyesha kuwa alianza maisha akiwa mchezadisko kwenye vilabu vya pombe na vingine. Baadaye alisoma na kuhitimu sheria mwaka 1961.

Biashara zake zimo katika maeneo kadhaa kuanzia kampuni ya ujenzi, televisheni kubwa ya Telemilano na nyingine mbili, kampuni ya uchapaji magazeti ya Giomele, redio, Shirika la habari la Rai pamoja na kumiliki klabu maarufu ya kandanda ya A.C.Milan.

Mwaka 1993 Berlusconi alianzisha chama cha siasa cha Forza Italia na kujitumbukiza kwenye siasa. Alitambua mapema kabisa kuwa ili aweze kufanikisha malengo yake; na hasa kukwepa mkono wa sheria kutokana na kufanya biashara nyingi haramu, ilikuwa muhimu kwake kuingia katika siasa – ili apate mahali pa kujikinga.

Njama hizo zilimsaidia sana Berlusconi kukwepa mkono wa sheria kutokana na makosa ya kukwepa kodi, udanganyifu, rushwa na  hata ngono. Kwa ufupi, maisha ya Berlusconi yamejaa mchanganyiko wa sifa na kashfa.

Alikuwa waziri mkuu wa Italia kwa vipindi vitatu, na mtawala aliyekumbwa na kashfa nyingi na hata kuhukumiwa kwenda jela. Lakini hakuwahi kutumikia jela kutokana na kujificha kwenye kichaka cha siasa.

Hata hivyo, baada ya kukwepa kwenda jela kutokana na makosa ya rushwa, ubakaji, kukwepa kodi na udanganyifu; hatimaye alijikuta akining’inizwa baada ya kutiwa hatiani na mahakama kwa kosa la kukwepa kulipa kodi mwaka 2013.

Kama hiyo haitoshi, alihukumiwa pia adhabu ya miaka saba jela kutokana na kufanya ngono na “kahaba” aliye chini ya umri wa mtu mzima. Adhabu hiyo, hata hivyo, ilibadilishwa na kuwa ya kutumikia jamii kwa mwaka moja kutokana na umri wake mkubwa – miaka 77.

Hiki kilikuwa kitu kipya kabisa kwa raia wa Italia ambao walifikia kuamini kwamba Silvio Berlusconi haguswi na mkono wa sheria kutokana na ukubwa kisiasa na utajiri wake.

Nchini Tanzania, wenye utajiri mkubwa walianza kwa kujipenyeza kwenye michezo kupitia vilabu vikubwa. Ukweli ni kwamba kelele za wanachama na mashabiki wa klabu, huweza kumsetiri mwizi na hata kuhakikisha kuwa hakabiliwi na mkono wa sheria.

Baada ya kugundua mbinu hiyo inafanya kazi, inawezekana sasa kuna waliojiingiza katika siasa, tena kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) au vyama vingine.

Siyo siri kwamba wizi na ufisadi wote uliotajwa hapo juu, umo nchini Tanzania. Siyo siri kwamba wizi mkubwa umewahusu viongozi wa serikali ambayo inaongozwa na CCM.

Siyo siri kwamba miongoni mwa wanaotaka kugombea urais, Oktoba mwaka huu, tena kupitia CCM, wamo watuhumiwa wakuu wa ama hujuma, wizi  au ukwapuaji mabilioni ya shilingi kupitia wizara ya fedha na BoT.

Ripoti ya hivi karibuni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa fedha za serikali (CAG); inaonyesha kuwa serikali inatumia vibaya fedha inazopewa; inapoteza fedha, na watumishi wake waliokabidhiwa dhamana kuu, wanatafuna fedha kama njugu kutoka shamba la bibi!

Ni kula! Kula! Kula! Ni kula faida na ziada; na hatimaye kula mbegu; kana kwamba mwakani hakuna kupanda!

Kinachostua wananchi wengi wapenda nchi yao, ni kuona waliotajwa na CAG – na huwataja mwaka hadi mwaka –  kuwa watuhumiwa ubadhilifu, wezi moja kwa moja, wakwapuaji na, au waandaa mipango ya uhujumu uchumi; ni miongoni mwa wanaotangulia kutangaza kugombea urais na ubunge.

Yuko wapi mwandishi wa kuwaanika hao? Yuko wapi mwandishi wa kuwahoji?

Kwa wizi wa waziwazi alioanika CAG, kuna wanaopaswa kuwa jela wakati huu au wakati wa uchaguzi, Oktoba. Serikali inayowaajiri, inayowakinga, inayostahili kuwafukuza au kuwakamata na kuwashitaki, iko kimya.

Ni serikali hiyohiyo ya chama hichohicho, inayotuhumiwa na kushutumiwa na CAG ambayo inasimamia upatikanaji rais kutoka miongoni mwa watuhumiwa  - Chama Cha Mapinduzi.

Katika mazingira haya, hakika hakuna kulala – kwa upande wa CCM na serikali yake. Wanataka kuhakikisha kuwa anapatikana mgombea na labda baadaye, rais atakayefunika kombe ili mwanaharamu apite.

Wanataka rais aendelee kutoka katika chama chao – CCM – kilichojaa viongozi wa serikali wanaotuhumiwa na kushutumiwa kwa wizi na ufisadi wa viwango mbalimbali; kuanzia kijijini hadi ikulu.

Wanataka kuendelea kujenga kinga kwa wahalifu wanaowafahamu, waliowaweka madarakani, waliowalea na watakaoendelea kulinda, kuhifadhi na hata kuenzi genge la wezi wa tunda la jasho na damu ya Watanzania.

Chama Cha Mapinduzi kinaweza kufananishwa na mtu mmoja aitwaye Robert Mugabe, rais wa Zimbabwe, ambaye aliapa kufia ofisini kwa hofu ya kukamatwa na kushitakiwa, pale tu atakapotoka ikulu.

Kuiba fedha za umma, kushiriki kuiba, kuruhusu kuiba na, au kunyamazia kuiba, ni kosa kubwa kimaandili, kisiasa na kisheria.

Wizi usioadhibiwa, au usiokemewa; na badala yake ukawa wizi wa kuendeleza kwa “gharama yoyote ile,” alimradi mtu amebaki madarakani; ndio unafanya vyama na watawala watake kufia madarakani; kama inzi anavyofia kwenye kidonda. Hawaoni usalama wao nje ya madaraka ya dola.

Watajipitisha makanisani, misikitini, misibani, kwenye harusi na matanga; wakijifanya wacha-Mungu na wenye kuwahurumia wasumbukao kwa njaa, maradhi na kiu; wakiwalaghai watu kwa vitenge, kanga, pilau au kofia za chama au ahadi za ajira, ili wapate kubaki madarakani.

Hakika, Watanzania wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuacha ngonjera za kuthamini “uasisi” na “kuleta uhuru.” Siyo siri kwamba vyama vilivyopigania uhuru Afrika na kwingineko, vingi viliingiliwa na kirusi cha wizi na ufisadi na hatimaye kuangushwa na umma.

Tanzania siyo kisiwa! Watanzania wanaona, kusikia na kunusa. Kama mwizi wa mali yao hakamatwi, basi wasiomkamata wasiwaombe kura ya kuendelea kutawala. Au wakiwaomba kura, basi wawakatalie.

CCM haikuundwa ili ilee wezi, iwatukuzwe na iwaweke madarakani. Hapana! Kwa kauli za Mwalimu Nyerere, iliundwa kulinda na kudumisha uhuru wa nchi na raia wake; kusimamia haki na maendeleo ya wakulima na wafanyakazi, kuhakikisha kuwa matumizi ya utajiri wa taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi, na hasa jitihada za kuondosha ujinga, maradhi na umaskini.

Kama walioahidi na wanaopaswa kuamini hayo ndio wenye serikali inayoanikwa na CAG kuwa ni badhilifu kupindukia; basi wameandika barua ya maombi kwa umma wakitaka kufukuzwa kazi. Watafukuzwa!

Kuwafukuza kazi ni kutowachagua; lakini kwanza ni kuwataka wagombea wao, hasa wanaotaka urais, kutaja walikopata fedha wanazomwaga misibani, michezoni, misikitini na makanisani; na jinsi watakavyozirejesha.

Isemwe tu basi, kwamba CCM bado ina nafasi ya kujisahihisha kwa kuwaengua wagombea urais, ubunge na udiwani – wote  wasio waadilifu – wahujumu, wezi, matapeli, walafi, wababaishaji na mafisadi.

Kama hilo litaigharimu kushindwa katika uchaguzi mkuu huu, isiwe hoja. Wakae pembeni. Wajipange upya na kurudi kwenye misingi walioyiacha, ndipo warejee kwenye kinyang’anyiro wakiwa wasafi na wenye sifa ya kushindana na hata kushinda.

*Lawrence Kilimwiko ni mshauri wa habari na mwandishi wa vitabu kutoka asasi ya Interlstar Consults, Dar es Salaam: lkilimwiko2015@gmail.com, Mob. 0754 321308.